KATIBU MTENDAJI WA BARAZA HILO, DK. CHARLES MSONDE.
Necta imesema haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wasimamizi hao wa mitihani pale udanganyifu wa aina yoyote utakapotokea.
Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alitoa onyo hilo jana, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mtihani huo ambao watahiniwa wa shule wanatarajiwa kuwa 323,513 na wa kujitegemea 62,425.
Dk. Msonde aliwataka wasimamizi wa mtihani huo kufanya kazi yao kwa uaminifu, uadilifu na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwa kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua.
"Udanganyifu umepungua," Dk. Msonde alisema, "mwaka 2011 watahiniwa waliofutiwa mitihani walikuwa ni 9,739, mwaka jana walikuwa 500."
"Watahiniwa hao walibainika kufanya udanganyifu kwa kuingia na simu, vitabu na notisi kwenye vyumba vya mitihani.
"Mwaka huu walikuwa ni watahiniwa 10 waliofanya hivyo. Hii ni dalili nzuri kuwa wanafunzi wanajiandaa vizuri."
Dk. Msonde pia aliwakumbusha wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha mitihani.
"Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa uwapo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya taifa," alisema.
Dk. Msonde alisema mitihani ya kidato cha nne na maarifa (QT) itafanyika kwa siku 19 kuanzia leo na utahusisha jumla ya shule za sekondari 4,787 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 1,064.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule 323,513 waliosajiliwa, wavulana ni 159,103 sawa na asilimia 49.18 na wasichana ni 164,410 sawa na asilimia 50.82.
"Watahiniwa 58 ni wasioona na watahiniwa wenye uono hafifu ni 305 ambao maandishi ya karatasi zao za mitihani hukuzwa. Mwaka jana idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa ni 355,822," alisema.
Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa wa kujitegemea 62,425 waliosajiliwa, wavulana ni 28,574 sawa na asilimia 45.77 na wasichana ni 33,851 (asilimia 54.23).
Alisema watahiniwa wa kujitegemea wasioona ni sita, kati yao wasichana ni watano na kwamba mwaka jana idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa ilikuwa ni 52,550.
Alisema jumla ya watahiniwa 16,279 wamesajiliwa kufanya mtihani wa maarifa (QT). Kati yao, wanaume ni 6,725 sawa na asilimia 41.31 na wanawake ni 9,554 sawa na asilimia 58.69 wakati mwaka jana idadi yao ilikuwa ni 20,655.
ENEO LA SHULE
Dk. Msonde pia alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika kwa amani na utulivu.
"Wananchi na waandishi wa habari wanaombwa kuheshimu eneo la mitihani," alisema. "Hairuhusiwi mtu yeyote asiyehusika na mitihani hii kuingia kwenye eneo la shule katika kipindi chote cha mitihani, hizi ni taratibu naomba ziheshimiwe."
Dk. Msonde aliwaasa walimu na watahiniwa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu kwa kuwa mtahiniwa atakayekamatwa, baraza litafuta matokeo yake.
"Watahiniwa wakumbuke kuwa mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa sababu inawapima uwezo na uelewa wao na matokeo ya mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa kujiunga na kidato cha tano pamoja na fani mbalimbali za utaalamu wa kazi," alisema.
Alizitaka kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji wa mitihani zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama na utulivu wa vituo vya kufanyia mitihani.
"Tumaanini walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi katika kipindi chote cha elimu yao ya sekondari. Ni matarajio ya baraza kuwa wanafunzi watafanya mitihani yao kwa kuzingatia kanuni za mitihani."
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando, alisema mkoa wake umejipanga kuhakikisha hakuna udanganyifu kwenye mitihani hiyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Ramadhan Kaswa, alisema anaamini mkoa wake utafanya vizuri kwenye mtihani wa mwaka huu.
Katika matokeo ya mwaka jana ya kidato cha nne, mkoa wa Lindi ulishika mkia kitaifa baada ya jumla ya watahiniwa wake 4,754 waliofanya 2,564 tu kufaulu kwa wastani wa GPA ya 4.3751. Mkoa huo ulishika nafasi ya 27 kwa matokeo ya mwaka 2015.
Dar es Salaam iliyowakilishwa na Mmbando, ilishika nafasi ya 18 mwaka jana baada ya watahiniwa 24,544 kati ya jumla ya 38,068 waliokaa kwenye dawati kupimwa kufaulu kwa wastani wa GPA ya pointi 4.1072. Mkoa huo ulianguka pia kutoka nafasi ya 15 mwaka uliotangulia.
Mikoa ya Njombe, Iringa na Kagera ndiyo iliyoshika nafasi tatu bora, kwa mpangilio wa mwaka jana.
Njombe iliyoshika nafasi ya 10 mwaka 2015 iliongoza mwaka jana baada ya wanafunzi 5,510 kati ya 6,181 waliofanya mitihani kufaulu kwa GPA ya pointi 3.7917
Iringa ilishika nafasi ya pili baada ya wanafunzi 9,598 waliofanya mtihani, 8,558 kati yao kufaulu kwa wastani wa GPA ya 3.7970. Mwaka 2015 mkoa huo ulikuwa wa tano kitaifa.
Kagera ambayo ilikuwa na watahiniwa 13,800 mwaka jana ilishika nafasi ya tatu baada ya wanafunzi 11,241 kufaulu kwa wastani wa GPA ya pointi 3.8569. Mkoa huo ulikuwa namba 12 mwaka 2015.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni